Saturday, April 15, 2006

KWA SABABU YOYOTE BADO BARAZA LA MAWAZIRI LA RAIS KIKWETE NI KUBWA MNO

Rais Kikwete ametangaza baraza lake la mawaziri na tayari limeapishwa na hivyo kuwawezesha mawaziri hao kuanza kazi kwa hari mpya,kasi mpya na nguvu mpya ili kujenga Tanzania yenye neema,baraza hilo lina jumla ya mawaziri 29, manaibu 31, ukijumulisha na waziri mkuu lina jumla ya mawaziri 61!.

Idadi hiyo kwa vyovyote vile ni kubwa mno si kwa kulinganisha na serikali za awamu zilizopita la hasha bali kwa kuchambua majukumu ya waziri na manaibu wao.

Swali la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza ni je,kulikuwa na umuhimu wa kuwa na wizara na manaibu wengi kiasi hicho? Majibu ya swali hili yatapatikana kwa kusoma makala hii,

Kwanza kuna wizara hii mpya ya Ushirikiano wa Afrika mashariki,wizara hii ina waziri na naibu wake! Pamoja na umuhimu wa jumuiya hii bado hakukuwa na sababu za msingi za kuwa na wizara kamili na naibu wake hata kama Kenya na Uganda wanazo wizara kama hii bado si sababu za msingi za wizara hii kuwepo,

Ushirikiano wa jumuiya (EAC) ni muhimu kwa maendeleo ya taifa letu la Tanzania na ukizingatia swala la utandawazi ndipo umuhimu unavyozidi kwani jamuiya yenye nguvu kiuchumi ndio itakuwa na sauti ulimwenguni..

Katika jumuiya ya Afrika Mashariki kinachotengenezwa ni mazingira na fursa ambazo zina tarajiwa zitumiwe na nchi wanachama wake, pale haukuti ajira, soko,wala vitega uchumi bali inatengenezwa fursa ya kuweza kutumika kuzarisha ajira, soko n.k, kwa maana hiyo wajibu mkubwa upo ndani ya nchi husika, mfano katika jumuiya na hasa tutakapokuwa tumefikia katika umoja wa soko(common market) ambapo raia wa nchi moja ataruhusiwa kwenda kufanya kazi katika nchi nyingine pasipo kuwekewa vizingiti na masharti yoyote, hii ni fursa ya ajira lakini haitakuwa na maana yoyote kwa Tanzania kama wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na wizara ya elimu ya juu,sayansi na teknolojia zitakuwa hazikujiandaa vyema kwa kuzarisha watanzania wenye ujuzi,maarifa na elimu ambayo inawafanya kuwa washindani katika soko(competitive), vivyo hivyo jumuiya ni fursa ya soko lakini Tanzania tutanufaika kwa kutumia soko hilo kwa kuwa na bidhaa bora zinazoweza kuuzika katika soko hilo na hapo ndipo jukumu la wazara ya uchumi, mipango na uwezeshaji,fedha. Pia na viwanda na biashara n.k zinapokuwa na umuhimu katika mchakato wa kuwawezesha watanzania kunufaika na fursa zinazopatika katika jumuiya

Kwa kuangalia mambo kama hayo yaliyotajwa utaona kuwa mambo ya msingi yanayotakiwa kutunufaisha sisi watanzania yanatakiwa yafanyike ndani ya nchi yetu na hayo ni makumu ya wazara mbali mbali kwa umoja wao, kutokana na sabubu hizo bado hakukuwa na hoja ya msingi ya kuwa na waziri kamili na naibu wake,wa nini? Kwa nini jukumu hilo lisingefanywa na naibu waziri katika wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa?
Katika hali halisi hivi sasa, nini yatakuwa majukumu ya kila siku ya wizara? Matokeo yake tutakuwa na watu ambao hawana majukumu ya kila siku hivyo kupoteza pesa na rasilimali kadha ambazo zingeweza kutumika sehemu nyingine ambazo ni nyeti zaidi,mfano katika jumuiya hii iliundwa mahakama ya Afrika Mashariki(The East Africa Court of Justice) lakini kipindi chote hiki tangu iundwe haijawai kupokea hata shauri moja,

Pili hakukuwa na sababu za msingi za kuwa na manaibu waziri wawili katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Kimataifa, izingatiwe kuwa mawaziri si watendaji wakuu wa wizara bali ni wasimamizi tu, kazi zote za kitaalamu za kila siku zinafanywa na wataalamu waliopo wizarani,kinachoitajika kufanyika hapo wizarani ni kubadilisha akiri (mindset) za watumishi ili wajue majukumu mapya ya wazara ya mambo ya nje ni kuiletea nchi shibe kwa kuitangaza vizuri na kuimarisha ushiriano wa nchi na nchi pia na vyombo na taasisi za kimataifa ulimwenguni,siasa za longo longo hazitailetea nchi shibe.

Waziri na naibu wake mmoja tu anatosha kutekeleza majukumu ya wizara hiyo,baadhi ya kazi za msingi za wizara hii zinaweza kutekelezwa vizuri sana na barozi zetu zilizoko nje ikiwa zitapangwa vizuri.

Tatu wizara ya mambo ya ndani imetenganishwa na kuwa wizara mbili moja ikiwa wizara ya usalama wa raia na nyingine ikibaki kuwa wizara ya mambo ya ndani na zima moto, ni kweli serikali ya awamu ya nne haipaswi iwaache majambazi yatambe kwa kuiba mali za wananchi na kuwaua, lakini kama serikali inafikiri sululisho la tatizo hili ni kuundwa kwa wizara ya usalama wa raia itakuwa imekosea na imepotea sana.

Kuongezeka kwa matukio ya ujambazi nchini kuna sababu nyingi tu za msingi na hazina uhusiano wa moja kwa moja na muundo na ukubwa wa wizara, kama vile Ukosefu wa vitendea kazi ndani ya jeshi la polisi ,si hajabu kukuta walaya nzima ina gari moja la polisi au mawili tu,idadi ndogo ya watumishi(polisi),mishahara na marupu rupu madogo yasiyojenga na kuongeza tija(productivity),ukosefu wa vifaa na zana za kufanyia kazi,udhaifu katika mbinu za kisasa na mikakati(strategy) za kukabiliana na wahalifu n.k hayo yote hayataondoka kwa kuunda wizara tu, ni mambo yanayojulikana ndani ya jeshi la polisi na watendaji wote waliokuwa wizara ya mambo ya ndani bali hayakutafutiwa ufumbuzi kwa sababu ukosefu wa bajeti ya kutosha.

Pia uhalifu umeongezeka kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi,tamaa ya kuwa na mali pasipokufanya kazi,mmomonyoko wa maadili,muingiliano wa jamii mbali mbali,utandawazi n,k ni vyema swala hili likaangaliwa kwa mapana yake, hii inanikumbusha kisa kimoja kilicho simuliwa na Mhudhama Karidinari Pengo ambaye anasema kuwa katika pita pita yake mtaani Dar es salaam aliwakuta akina dada wanafanya biashara ya ngono(umalaya) alisimamisha gari na kuwauliza kuwa nyie hamuoni kuwa mnahatarisha maisha yenu kwa UKIMWI? Kina dada hao walimjibu kuwa ni heri kufa na UKIMWI kesho kuliko kufa na njaa leo, ninachotaka kueleza ni kuwa ni vyema tuka angalia sababu za msingi(root cause) za kuongezeka kwa uhalifu na tukapambana nazo badala ya kuangalia matokeo tu, sabubu hizo hizo ndizo zinapunguza ufanisi katika magereza,uhamiaji na zimamto n.k
Nne hakuna sabubu ya kuwa na waziri anaye shughulika na mazingira peke yake labda kama ni kuwafurahisha wafadhili na hivyo kuvutia misaada , kwa maoni yangu waziri mmoja tu angetosha kushughulikia, mazingira na mambo ya Muungano ,kwani ukiangalia kwa undani shughuli zote za uharibifu wa mazingira zinafanyika katika wizara mbali mbali, mfano kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika uchimbaji na usafishaji wa madini,Kilimo,Mifugo,Maji ,Mali ya asiri na Utalii,Makazi,Miundo mbinu n.k vivyo hivyo ni jukumu la wizara husika kuhakikisha kuwa shughuli zilizoko chini ya wizara husika zinalinda na kujenga mazingira kwa faida ya kizazi cha leo na kesho.

Pia Mambo ya Muungano yote yana wizara zinazowajibika kwa kila siku juu ya maswala ya muungano kama vile Wizara ya Fedha,Elimu ya juu,sayansi na teknolojia, Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa, Mambo ya nje na Ushirikano wa kimataifa, mambo ya ndani n.k ninachotaka kukieleza hapa ni kuwa shughuli zote zinazo husu muungano zina waziri muhusika anayewajibika nazo kila siku,

Kutokana na sababu hizo hakukuwa na haja ya kuwa na mawaziri wawili bali waziri mmoja tu angetosha kushughulikia mazingira kama mratibu tu na muunganishi wa wizra zote ili kuhaikikisha zinalinda mazingara pia vivyo hivyo angeweza kuratibu na kuwa kiunganishi ili kuhakikisha kuwa wizara husika zinatekeleza majukumu yao kulingana na mkataba wa muungano,Katiba na sheria za nchi zinazo husu muungano,kama nilivyoeleza hapu juu shughuli zote za kila siku zina mawaziri husika hivyo kumfanya waziri huyu kuwa na majukumu madogo ambayo anaweza kuyaghulikia yote mawili yaani mazingira na muungano.

Tano hakukuwa na sababu ya msingi kuwa na naibu waziri anayeshughulikia maafa na kampeni ya UKIMWI, shughuli za kampeni ya UKIMWI zinaweza kufanywa vizuri na wizara ya afya kama inavyofanya kwa magojwa mengine kama vile maralia,kipundu pindu,kisukari,Tb n.k,kweli ukimwi ni hatari, na maali pake ni wizara ya afya lakini pia ni ukweli ulio wazi kuwa maralia inaua watu wengi kuliko ukimwi inakadiriwa kuwa kila baada ya dakika Watanzania 5 wanakufa kwa maralia sasa kama ni kujali maisha ya watanzania basi maralia ndio ilipaswa kupewa naibu waziri. Naibu anayeshughukia bunge angeweza pia kushughulika maafa pasipo kuathiri ufanisi wa kazi.

Sita hakuna sababu ya kuwa na mawaziri wa nchi wawili mmoja akishughulikia Utawala bora na mwingine akishughulikia Siasa na uhusiano wa jimii,kimantiki yote hayo ndio utawala bora kwahiyo yange uganishwa na kuwa chini ya waziri mmoja,

Saba sioni sababu za msingi za kuwa na wizara ya kazi, ajira na maendeleo ya vijana na kuwa na manaibu wawili, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa hapo mwanzo shughuli za wizara hii nyingi zinafanyika au kutekelezwa katika wizara nyingine , wizara hii imewekwa kisiasa mno, si jukumu na wala haitarajiwi wizara hii kuzarisha nafasi za kazi kwa watanzania, maana nafasi za ajira zitapatikana kwa uchumi kukua,viwanda kuazishwa,kilimo na mifugo kuboreshwa n.k hivyo shughuli haswa za kuzarisha ajira zipo katka wizara nyingine,pia vivyo hivyo maendeleo ya vijana kwa maana pana ,ni kupata elimu bora,ajira, afya safi na kwa ujumula maisha yenye neema na mambo yote hayo yanafanyika na kutekelezwa na wizara mbali mbali kwa ujumla wake,
Jukumu la kubuni sera,kutunga sheria na kusimimia sheria ya kazi yanaweza kutekelezwa kwa baadhi kuyahamishia wizara ya habari,utamaduni na michezo na mengine kuwa ni idara tu katika wizara nyingine.

Nchi hii ni yetu sote na tunalo jukumu la kutoa mawazo juu ya msakabali wa nchi yetu,ni mawazo dhaifu kusema kuwa tusubiri kwanza ili tuone utendaji wa baraza ndio tutoe maoni,hii ni falsafa mbaya ya kusubiri janga litokee ndiyo uanzae kulishughulikia ,waswahili usema heri nusu shari kuliko shari kamili,mimi kama mtanzania niliyebahatika kusomeshwa na nchi yangu ninao wajibu wa kuchangia mawazo juu ya ujenzi wa nchi yetu, mawazo haya siyo lazima yawe sahii kwa asilimia mia bali ni jukumu la kila mwananchi kuchangia mawazo juu ya maendeleo ya nchi yetu Tanzania, Nawatakia afya, fikra mpya za kuigeuza Tanzania kuwa yenye neema.

1 Comments:

Blogger Ndesanjo Macha said...

Ndugu Kahwa, karibu sana. Nafurahi kusikia kuwa makala kuhusu kublogu zilikugusa. Naamini kuwa nawe kwa kutumia safu yako na blogu yako na mtandao ulionao (marafiki, ndugu, majirani, n.k.) utagusa wengine wengi.

12:25 PM  

Post a Comment

<< Home