Sunday, April 16, 2006

MKUU WA JESHI LA POLISI ANAPOTOA TUHUMA KWA MSINGI WA HISIA!

Nchini Tanzania tumezoea kuwasikia wanasiasa wakitoa tuhuma mbali mbali juu ya wapinzani wao wa kisiasa pasipokuwa na ushahidi wowote na wanapobanwa ujitetea kuwa hizo zilikuwa ni kauri za kisiasa kana kwamba wanasiasa wameruhusiwa kufanya hivyo! Tabia hii ya kutoa tuhuma nzito imeonekana kuwa ni mtindo kwa watanzania wengi na inaonekana rais mstaafu W. Mkapa hakupendezwa kabisa na mtu yeyote kumtuhumu mwenzake pasipo kuwa na ushahidi na mara kwa mara alikemea swala hilo na alisisitiza umuhimu wa tuhuma kuambatana na ushahidi.


Ukiangalia majukumu ya jeshi la polisi kwanza ni kuhakikisha kuwa sheria na taratibu za zinalindwa (maintain law and order), ni jukumu la jeshi la polisi kuhakikisha kuwa sheria zilizo tungwa na bunge letu zinatekelezwa na wananchi wote pasipo kubagua mtu yeyote,jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine na wananchi kwa ujumla ujitahidi sana kuhakikisha kuwa sheria na taratibu zinafuatwa kwa faida ya watu wote na hivyo kuifanya nchi kuwa mahali salama pa kuishi na kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo ya taifa letu.

Pili Jeshi la polisi limekasimiwa majukumu ya kulinda maisha ya raia na mali zao(protection of life and property) hivyo ni jukumu la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine kuhakikisha maisha na mali za wananchi wa Tanzania ziko salama , hivyo ni jukumu la polisi kuhakikisha kuwa vitendo vya ujambazi ambavyo vinaonekana kuongezeka kwa kasi hivi karibuni na kusababisha mali na maisha ya watanzania kuwa hatarini vinapunguwa kama si kuondolewa kabisa.

Tatu ni kugudua vitendo vya uhalifu (detection of crime), kukamata(arrest),kuedesha mashitaka, usalama barabarani,kulinda sera za nchi (safeguard the policy of the country) na ni jeshi la akiba, hayo ndiyo majukumu ya jeshi la polisi kimsingi,

Kwa nujibu wa sheria jeshi la polisi halipaswi kwa njia yoyote kushabikia au kuwa mpenzi wa chama fulani cha siasa, pia polisi wakiwa kama watumishi wa chombo cha dola hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.


Makala hii ni matokeo ya matamshi ya mkuu wa jeshi la polisi afande Omary Mahita kama alivyo kaririwa na vyombo vya habari hapa nchini kuwa Chama cha CUF kinahusika na vitendo vya ujambazi hapa nchini! pia kuwa yeye akiwa mkuu wa jeshi la polisi chama cha CUF akitaingia madarakani mpaka kiama!

Baada ya kusoma magazeti kadha na kumsikia katika televisheni nimejiuliza maswali kadha na kuamua kuandika makala hii.

Kwanza nani kampa madaraka Mahita ya kuchagua chama cha kuingia madarakani?kutokana na sheria ya uchaguzi ,rais ,wabunge na madiwani uchaguliwa na wananchi wa Tanzania kwa kupigiwa kura ya siri,na ni Tume ya Uchaguzi ya Taifa yenye mamlaka ya kumtangaza mtu kuwa rais,mbunge na diwani sasa Mahita nguvu za kusema kuwa chama cha CUF hakitaingia madarakani mpaka kiama anazitoa wap?, kwani kwa kuangalia majukumu ya jeshi la polisi kama nilivyoyataja hapo juu hakuna kifungu kunachompa mamlaka hayo, pia ukisoma sheria ya uchaguzi hakuna kifungu kinacho mpa madaraka hayo ,sasa ni jambo la kushangaza kumsikia kiongozi mkubwa wa jeshi la polisi kama yeye akitoa maneno kama hayo, pia kwa mujibu wa sheria ya usajiri wa vyama vya siasa, chama usajiriwa na msajiri wa vyama vya siasa baada ya kukidhi matakwa ya sheria ya vyama, na chama chochote kilichosajirwa kinayo haki kisheria kushiriki katika uchaguzi na kuomba ridhaa ya kuongoza nchi toka kwa wapiga kura na si kwa afande Mahita..

Kuongezeka kwa vitendo vya ujambazi kwa siku za karibuni kusiwe chanzo cha kuleta vurugu nchini, viongozi bado wanapaswa kutambua kuwa nchi bado inaendelea kutawaliwa kwa kufuata katiba na sheria mbali mbali za nchi hii.

Katika sheria za nchi sidhani kama kuna kifungu kinachomuhalalisha mkuu wa jeshi la polisi kukituhumu chama au mtu yeyote kwa kutumia hisia! Mahita amekaririwa akisema kuwa anahisi kuwa vitendo vya ujambazi vinavyofanyika hivi sasa ni hujuma inayoandaliwa na chama cha CUF! Hapo ndipo ninapo pata tatizo kumuelewa afande wa jeshi la polisi.

Kwanza yeye hakupaswa kulalamika na kuutangazia umma wa watanzania juu ya hisia zake, kwani kwa mujibu wa uchunguzi kama taaluma agezifanyia kazi kwanza hisia zake kwa kuamru upelelezi kufanyika ili kukusanya ushahidi wa hisia zake na baada ya kujiridhisha na ushahidi alioukusanya angewakamata na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa na siyo kukimbilia kwenye vyombo vya habari,tatizo la Mahita anakuwa mwanasiasa zaidi kwani ni tabia ya wanasiasa wengi ulimwenguni kupenda kuonekana katika vyombo vya habari pasipo kuwa na sababu za msingi, tangu lini jeshi la polisi likawa linatangaza hisia za mtu na kuwambia watuhumiwa kuwa najiandaa kuja kuwapekuwa! Hivi hata kama ingekuwa kweli viongozi wa CUF kuwa wanashirikiana na majambazi, je taaluma ya upelelezi inamtaka Mahita awatangazie kwenye vyombo vya habari kabla ya kuwapekuwa na kuwakamata? Hii si ndiyo kuwapa nafasi ya kuficha silaha na ushahidi mwengine ambao ungekuwa muhimu kuthibitisha tuhuma?

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana Disemba Mkuu wa jeshi la polisi alikaririwa na vyombo vya habari akikituhumu chama cha CUF kuwa kilishiriki kuingiza visu vyenye rangi na nembo zinazotumika na chama hicho lakini ni jambo la kushangaza kuwa hatujasikia mpaka hivi sasa ni watuhumiwa wangapi wamefikishwa mahakamani kwa kuingiza nchini visu kama hivyo,je watengezaji wa visu hivyo wamehojiwa na kukiri kuwa visu hivyo viliagizwa na CUF,je vililipiwa ushuru bandarini,uwanja wa ndege au mpakani? Je maofisa forodha waliovikagua visu hivyo wamehojiwa, Je unatofautishaje swala la chama na mwanachama au mpenzi binafsi? n.k hayo ndiyo mambo ya msingi ambayo Mahita angetakiwa kuyafanyia kazi kabla ya kukimbilia katika vyombo vya habari,

Inapotokea mkuu wa jeshi la polisi anaendesha jeshi kupitia katika vyombo vya habari hapo ndipo uwezo na mbinu za mkuu huyu vinapotia shaka sana, kufoka na kutumia lugha kari si mbinu wala mkakati muhususi wa kupambana na uhalifu nchini, hizo ni mbinu za mwaka 1940s, dunia ya sasa haitaji makeke bali ni mbinu za kisayansi zaidi na pengine ukimya zaidi unaonekana kufanya kazi, wananchi wanapenda kusikia watuhumiwa wakiwa wamefikishwa mahakamani na ushahidi.


Vitendo vya ujambazi vinavyofanyika hapa nchini vanatumia bunduki na siyo visu ambavyo Mahita amekazania kuvionyesha, na hata kama ingekuwa ni visu tanataka wahusika wafikishwe mahakamani na siyo kuishia kuonyesha visu katika televisheni mbona watuhumiwa hawakuonyeshwa!

Si nia ya makala hii kukitetea chama cha CUF la hasha bali nasisitiza umuhimu wa mkuu wa jeshi la polisi kufuata sheria na taratibu za nchi hii, hivyo ndiyo utawala bora unavyotaka mambo yaendeshwe , Bila kuingia ndani, vitendo vya ujambazi mitaani,katika mabenki,kwenye magari, na mahali popote havichagui chama Fulani, mfano wizi wa NBC LTD huko Moshi,CRD LTD Tawi la Azikiwe Dar es salaam,NBC LTD Ubungo,Uporaji katika duka la vito Kariakoo,Wizi katika duka la kuuza fedha za kigeni nk Pia majambazi yamekuwa yakifanya uhalifu sehemu mbali mbali za nchi kama vile huko katika msitu wa Bihalamulo,Ngara,Karagwe, Kigoma, Mwanza, Arusha, Mbeya ,n.k huko kote majambazi yaliua na kupora mali za wananchi mbali mbali pasipo kuuliza uanachama wa chama chochote, majambazi wanaweza kutoka katika chama chochote kiwe cuf,ccm,chadema tlp n.k na wanapoamua kuua au kupora hawangalii uanachama wa ntu yeyote wao wanachotaka na fedha na mali tu.

Inaonekena Afande Mahita kaishiwa mbinu za kukabiliana na changamoto zinazolikabili jeshi la polisi kwa hivi sasa na anatafuta mbinu rahisi na hatari ya kuhusisha ujambazi na siasa za vyama na kwa njia hiyo anafikiri ataweza kuungwa mkono na wabunge,madiwani na serikali iliyoko madarakani!

Kama Mahita anafikiri hivyo atakuwa amapotea na amekosea sana, hakuna anayeweza kukubaliana na hoja dhaifu kama zake, wananchi kwa ujumla hawako tayari kukubaliana na sentesi za kiujulma kama zake,Pole sana Mahita hakuna aliye tayari kuingia katika mtego wako,dunia ya sasa watu hawaburuzwi na kauri za viongozi,dunia ya sasa inawapa nafasi wananchi kufikri na kutafakari kwa kina kabla ya kumuunga mkono mtu.

Kauri ya Afande Mahita imelihabisha na kuridhalilisha jeshi la polisi mbele ya umma wa watanzania, jamii haikutarajia kiongozi wa chombo kikubwa kama jeshi la polisi kutoa kauri ya kiujumla jumla kama yake.

Afande Mahita aelewe kuwa inawezekana kuwa sauti,muonekano, makeke n.k ya kupambana na uhalifu bado anavyo na vinazidi kuongezeka kila kukicha lakini ni ukweli ulio wazi kuwa akiri,mikakati, mbinu za kupambana na ujambazi vinaonekana kupungua kadri siku zinavyokwenda, jamii haina uwezo wala nguvu za kisheria za kumwambia ajiuzuru lakini ukweli unabaki pale pale kuwa sifa za kuendelea kuitwa mkuu wa jeshi la polisi Tanzania zinaonekana kupungua kwa kasi ya ajabu sana.


Huu ni mchango wa mawazo kwa kauri ya mahita.Makala hii ilitoka katika gazeti la Tanzania daima
innokahwa@yahoo.com

0 Comments:

Post a Comment

<< Home