Sunday, April 16, 2006

WAPIGA DEBE SERIKALI ILICHELEWA SANA KUWACHUKULIA HATUA

Kumekuwepo mjadala juu ya wapiga debe katika vituo vya daladala hususan jiji la Dar es salaam,kuna maoni tofauti wengine wakiunga mkono kuondolewa kwao na baadhi wakipinga, ,kwa wale wanaopinga kwa kuwa wanatumia uhuru wao wa kikatiba sawa, lakini hakuna mtumiaji wa usafiri wa daladala atakaye pinga kuondolewa kwao, inawezekana wale wanaoipinga serikali hususani jiji kuwaondoa si watumiaji wa usafiri wa umma.

Ni kweli kuwa hivi sasa Tanzania inatekeleza sera ya soko huria lakini ikumbukwe kuwa biashara huria siyo leseni ya kuwafanya watu waishi bila kufuata sheria na taratibu za nchi au miji na majiji, pia ni kweli kuwa nchi inakabiliwa na janga la ukosefu wa ajira miongoni mwa wananchi wake hususan vijana lakini hiyo siyo sababu ya kuhalalisha wapiga debe vituoni, kwani wapiga debe ni wahalifu kama wahalifu wengine na hawawezi kuhalalishwa kwa kisingizio kuwa wanatafuta pesa za kujikimu.

Duniani wakati wa kampeni vyama ujinadi kwa kuahidi kutatua matatizo kadha yanayoikabili nchi husika kama vile ,tatizo la ajira,rushwa,uchumi, mazingira,uhalifu,n.k hakuna chama chochote makini kitakacho jinadi bila kueleza kuwa iwapo kitachaguliwa na kuingia madarakani kitatatua matatizo kama hayo, tumeshuhudia hata kwetu vyama vyote vilieleza matatizo kam hayo na hususan ajira kikiwemo chama cha mapinduzi.

Pia ni vyema jamii ikaelewa kuwa tatizo la ajira ni tatizo lililopo dunia nzima ,tofauti iliyopo ni aina ya ukosefu wa ajira baina ya nchi na nchi,na hakuna serikali duniani iliyomaliza kabisa tatizo la ajira la hasha bali kinachofanyika ni kulipunguza, si nia ya makala hii kukubaliana na hali iliyopo hivi sasa bali nia yangu ni kulieleza tatizo na kulijua na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana nalo.

Ni kweli chama cha mapinduzi kiliahidi kuwa kitaongeza nafasi za ajira zipatazo milioni moja,kuna wanao beza kuwa haiwezekani ni uhuru wao kufanya hivyo lakini ni vigezo gani wanavitumia kubeza sijui,tunahitaji vigezo vya kitaalamu na wala siyo, hisia, kwa kuangalia Tanzania,maliasili,jiogorafia yake inapakana na nchi nane, bahari,idadi ya watu,utulivu wa kisiasa,utengemavu wa uchumi mkuu nk naona kuna uwezekano wa kuwa na nafasi zaidi ya hizo zilizotajwa na ccm.

Kwa watu makini ineeleweka kabisa kuwa kupatikana kwa nafasi za kazi ni mchakato na siyo swala la siku moja tu na wala haitarajiwi nafasi kama hizo ziwe zile za kuajiriwa serikalini,serikali inachotakiwa ni kujenga mazingira na fursa hivyo ni jukumu la mtu binafsi kutumia fursa hizo na hapa izingatiwe kinachotakiwa ni fursa halali.

Ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi yetu tuna amini kuwa ni jukumu la serikali kukufanyia kila kitu kana kwamba serikali ina uwezo wa kimiujiza,

Ukiangalia wapiga debe wa mjini Dar es salaam hususan hawa wa vituo vya daladala, hakuna mtu makini anayeweza kuwaunga mkono wawepo kwa hali kama ilivyo hivi sasa, kwanza hawatakiwi na hawakubaliki na makondakta na madereva wa daladala na hvyo malipo yao ni ya kulazimisha yakiambatana na vitisho,ubabe na vurugu za kila aina, muulize dereva au kondakta yeyote juu ya watu hawa utapata jibu, kesi kadha zimeripotiwa katika vyombo vya habari juu ya kuchomana visu na wakati mwingine kuuana wakati wa kudaina malipo, kaulize kwa chama cha wenye daladala juu ya watu hawa,pia ni kero na wasumbufu kwa wasafiri na mwisho hakuna chombo chochote kinachowatambua bali wanalazimisha tu.

Kinachoitwa ajira ya wapiga debe mjini hakikubaliki hii siyo ajira ,ajira lazima iwe halali na lazima pawepo na makubaliono ya hiyari kwa pande zote, kwanza ni kuongeza gharama za uendeshaji bila sababu za msingi hebu angalia mfano ufuatao, abiria anaamuka asubuhi anaenda katika kituo cha daladala cha Rozana kilichopo Buguruni ili akapande daladala la kwenda Posta au Kariakoo pale kituoni anakuta msululu wa abiria wakisubiri basi na linapofika wanasukumana na kugombea ili kuweza kuingia ndani na kupata nafasi na siyo kukaa maana kukaa wakati wa asubuhi ni anasa sasa katika mazingira kama hayo mpiga debe wa nini na analipwa kwa kazi gani, maana kwa wakati huo magari ni machache kuliko abiria lakini utaona kundi la wapiga debe kibao! hii ndiyo tunaita ajira?

Si hivyo tu bali hata wakati wa mchana ambapo abiria wanakuwa wachache na magari kuwa mengi bado wapiga debe hawahitajiki maana kazi ya kuvutia abiria inaweza kufanywa na deriva pamoja na kondokta wake, kinachohitajika ni hawa makondakta na madereva kupewa semina ili kujua abc za uendesahji wa daladala ,napendekeza chama cha wanye dala dala waendeshe semina za kuwaelimisha madereva na makondakta na hivyo kuwafanya waweze kuendesha kistarabu zaidi na kwa gharama nafuu, maana wakati mwingine gharama za uendeshaji zinaongezwa na ukosefu wa elimu ya msingi ya biashara ya daladala, gharama zinazotokana na faini,rushwa,ajali,uharibifu wa gari na kuchakaa mapema,gharama ya wapiga debe n,k vyote hivyo vinaweza kuepukwa na hatimaye kumpunguzia abiria gharama za usafiri.

Kwa kuwa na waedeshaji wenye elimu ya biashara ya daladala hakuna haja ya kuwa na wapiga debe kwani kazi hiyo itafanywa na kondakta na dereva, mfano wakati wa asubuhi kondakta anaweza kutumika kuwapanga abiria ili wapande gari kwa kufuata utaratibu maalumu wakati huo kukaanzishwa utaratibu maalumu wa mabasi kuegesha vituoni na kutakiwa gari la kwanza ndilo linaanza kupakia(first in first out) na vitu kama hivyo.

Nchi zote ulimwenguni zina matatizo yanayotofautiana kutokana na tofauti ya maendeleo,mazingira,tamaduni,historia n,k na ni kweli kuwa matatizo ni zao la jamii husika,lakini pia kuishi ni mchakato ambao uzaa na kuibua matatizo kulingana na wakati, hivyo ni jukumu la jamii kushughulikia tatizo kadri linavyojitokeza.

Tatizo nilionalo na ambalo rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin W.Mkapa aliwahi kuligusia ni kuwa kuna hatari ya kujenga taifa la walalamishi tu,wachambuzi wengi wamekuwa wepesi wa kulaamu tu tena ni hodari sana lakini kulaumu siyo sululisho ni vyema tukawa tunalaumu na kutoa sululisho.

Katika kutatua tatizo kuna hatua kuu zifuatazo kwanza ni kuhainisha tatizo(problem identification) hapa tuna tatizo la ajira mjini na vijijini,wapiga debe ni matokeo ya tatizo la ajira kwa upana wake, hivi sasa mijini kuna vijana ambao hawana ajira na matokeo yake wanatafuta njia rahisi ambazo wanafikiri kuwa ni ajira mfano,wapiga debe,machangu doa,majambazi,n,k kumbe hizo siyo ajira bali ni uhalifu kama uhalifu mwingine ambao unaadhibiwa mbele ya sheria,jambazi hawezi kuhalalisha ujambazi wake kwa kisingizio kuwa serikali haijampatia ajira na hana njia nyingine ya kuweza kumfanya aweze kujikimu kimaisha,vivyo hivyo kwa wapiga debe hawatikiwi na wenye magari,hawatikiwi na abiria na mwisho jiji haliwatambui kwahiyo ni vyema wapiga debe tuwaangalie kwa mtazamo huo.

Hatua ya pili ni kuangalia njia mbadala(alternatives solutions) za kuweza kuondoa tatizo husika,hapa kuna njia kuu mbili kuna zile za muda mrefu kama vile MKUKUTA,MKURABITA,MMEM,MMES,urekebishaji wa uchumi,ujenzi wa vyuo vikuu na vya ufundi ,ukaribishaji wa vitega uchumi,uhanzishaji wa viwanda vidogo vidogo na vikubwa,ujenzi wa miundo mbinu n,k, pia kuna njia za muda mfupi kama vile kuwaelimisha wapiga debe ili wajue kuwa vitendo vyao siyo ajira bali ni uhalifu,kuwaondoa,kuwapatia mashamba, kuwahimiza wajiunge katika vikundi vya uzarishaji mali, kuwapeleka katika mafuzo mbali mbali ,kuwaingiza katika mfumo rasmi na hivyo kutambuliwa kwa kazi yao kama ajira na washika dau wa usafiri mijini na hvyo kazi hiyo kuendeshwa kwa utaratibu maalumu wenye kuelewaka na usiyo na kero kwa pande zote n.k

Hatua ya tatu ni kuchagua njia muafaka (selecting best alternatives) kati ya zilizo tajwa katika hatua ya pili, hii inategemeana na rasilimali zilizopo,ukubwa wa tatizo,muda , uharaka, mazingira n.k

Hatua ya nne ni utekelezaji(implementation), njia zilizoteuliwa kutatua tatizo utekelezwa, na hapa ndipo ujitokeza watu wengi wa kulaumu utekelezaji pasipo kutoa njia mbadala ambazo wanafikiria kuwa nzuri zaidi.

Hatua ya mwisho ni mshindo nyuma(feedback) baada ya utekelezaji ni vyema ikafanyika tathimini ili kujua kwa kiasi gani tatizo limeweza kutatuliwa na kama la kwa nini?.

Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa swala la wapiga debe kama matatizo mengine lililvyoachwa kwa muda mrefu bila kushugulikiwa na linaposhugulikiwa inakuwa siasa mno,inawezekana jamii ilishaaza kuliona kuwa ni jambo la kawaida ,mazoea yana taabu, Mfano kuna wizi wa vifaa vya magari kama vile tairi,vioo,radio,taa nk ambao ufanyika Dar es salaam na vifaa hivyo kupelekwa kidongo chekundu(gerezani) ambapo mwenye kifaa kilicho ibiwa utakiwa kukinunua tena kifaa chake kutoka kwa wezi au mawakala wa wezi hao na unapojaribu kutoa taarifa polisi kama ni kioo kinaweza kuvunjwa mbele ya macho yako na hakuna hatua zinazochukuliwa na imefikia hatua ya wenye magari kuona hilo ni jambo la haki na la kawaida na hivyo mtu kununua kifaa chake ni jambo la kawaida,sijui kwa siku za karibuni na hasa kasi mpya kama hali imebadilika lakini ninachotaka kueleza kuwa kuna hatari jamii ikikata tamaa na kuzoea uhalifu na kuona wa kawaida ,serikali ilichelewa kuchukua hatua dhidi ya wapiga debe na hatua zilizochukuliwa ni muafaka za kuwaondoa.

Makala hii iliwahi kutoka katika gazeti la Tanzania daima
innokahwa@yahoo.com
Tel +255744292718

0 Comments:

Post a Comment

<< Home